KUTOKANA na usajili waliofanya na ubora wa kikosi kwa msimu wa 2023/24, mashabiki wa Simba wameomba kupewa sumu ikiwa tu timu hiyo haitatinga hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ikumbukwe kwamba msimu wa 2022/23 watani zao wa jadi Yanga walitinga hatua ya fainali katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Pia mgeni rasmi, Rais Samia Suluhu aliweka wazi kuwa anatambua mafanikio ya Simba kugotea hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kufika hatua ya fainali.
Samia aliongeza kuwa ni muhimu timu zote kushirikiana iwe ni Simba, Yanga, Azam FC na Singida Fountain Gate inapofika suala la mashindano ya kimataifa.
Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Robertinho Oliveira inashiriki mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, (CAF) msimu wa 2022/23 iligotea hatua ya robo fainali.
Katika kilele cha Simba Day, Agosti 6 miongoni mwa mabango ya mashabiki yaliyozua gumzo ni pamoja na lile lililosomeka namna hii: “Kwa Simba hii tusipofika nusu fainali Club bingwa nipewe sumu nife.”
Miongoni mwa wachezaji ambao wapo ndani ya kikosi cha Simba msimu ujao ni Luis Miquissone, Clatous Chama, Kibu Dennis, Shomari Kapombe na John Bocco.