ALLY Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga, ameweka wazi kuwa, kwa msimu mpya wa 2023/24, malengo yao ni kuendelea pale walipoishia msimu wa 2022/23.
Msimu wa 2022/23, Yanga ilikomba taji la Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii na Kombe la Azam Sports Federation, huku ikigotea nafasi ya pili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Kamwe amesema wanahitaji kufanya vizuri zaidi msimu ujao kwa kutwaa mataji yaliyopo mikononi mwao ikiwa ni kama biti kwa watani zao wa jadi Simba ambao nao mpango wao ni kutwaa mataji hayo.
Kamwe kuhusu msimu wa 2023/24, Kamwe amesema: “Ni msimu ambao utakuwa na ushindani mkubwa, kila mchezaji anatambua ambacho tunahitaji ni kuendelea pale tulipoishia, hivyo tunahitaji mataji na kufanya vizuri kwenye mashindano tunayoshiriki.
“Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika tunahitaji kufika mbali, lakini kwa kuanzia malengo ni kuona tunaanzia hatua ya makundi, kisha tutaendelea na mipango mingine kwani kila hatua ni muhimu kwetu.”.
Yanga itamkosa Fiston Mayele ambaye amejiunga Pyramids ya Misri ni yeye alifunga mabao mawili kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
Katika mchezo huo langoni alikaa Beno Kakolanya ambaye kwa sasa ni mali ya Singida Fountain Gate.