SEKTA YA SKAUTI INAHITAJI MABORESHO BONGO

KWENYE upande wa usajili kumekuwa na sarakasi nyingi kwa timu za Bongo iwe kuanzia Ligi ya Wanawake, Championship mpaka Ligi Kuu Bara.

Sio Simba, Yanga mpaka Geita Gold kumekuwa na sarakasi nyingi ambazo zinachezwa.

Mpaka Namungo pia nao Singida Fountain Gate wanatambua namna ambavyo wamekuwa wakipambana kwenye upande wa masuala ya usajili hivyo ni muhimu kuwa na maboresho.

Haya yote yanatokana na umakini mdogo kwenye masuala ya usajili wa wachezaji wapya hasa kwenye kitengo cha kufuatilia wachezaji.

Ipo wazi kwamba kuna wachezaji ambao huwa wanapewa kandarasi wakiwa na uwezo wa chini kuliko wale ambao wapo kwenye kikosi husika kinachowasajili.

Na wakati mwingine kumekuwa na wachezaji wenye ubora mkubwa wanaachwa kisha wale ambao wanakuja kuchukua mikoba yao uwezo wao unakuwa wa kawaida.

Kufikia maendeleo kwenye usajili wa wachezaji ni muhimu dawati la skauti kwa timu za Bongo likafanyiwa maboresho na kuongezewa nguvu.

Hakuna mchezaji anayesajiliwa kwa kuonekana kwenye mchezo mmoja ni mwanzo wa kufelishana kwenye mechi za ushindani.

Kwa kila mchezaji anayetambulishwa ndani ya timu ni muhimu kila sekta kujiridhisha na aina ya mchezaji pamoja na benchi la ufundi.

Wale wataalamu ambao wanafuatilia ubora wa mchezaji ni muhimu kujiridhisha kwa kiwango kikubwa kuhusu ubora wa mchezaji pamoja na maendelezo yake kwenye upande wa afya.

Kuumia ni sehemu ya mchezo lakini wapo ambao huwa wanakuwa ni wagonjwa kwa muda mrefu hawa ripoti zinapaswa kuwepo mapema mezani kabla ya kupewa dili jipya.

Ukweli ni kwamba kumekuwa na mipango mingi nje ya ripoti kwenye usajili wa wachezaji wapya huku wale ambao wanapewa jukumu la kufuatilia uwezo wao nao wakiwa ni miongoni mwa wanaoruhusu haya kutokea.

Wakati mwingine inaweza kuwa shinikizo kutoka kwa viongozi ama presha kubwa kutokana na kushindwa kufuatilia mchezaji kwa muda mrefu.

Ili kupata wachezaji wazuri ni muhimu kila sekta ikafanya kazi yake kwa umakini kwenye kufuatilia kila jambo masuala ya kuingiliana majukumu ama kupeana kazi kwa kujuana yasipewe nafasi,

Mashabiki wa timu zote iwe ni Simba, Yanga, Kagera Sugar wanapenda kuona wachezaji ambao wanaletwa wanakuwa imara na kuonyesha kile kinachostahili.