SIMBA YATEMBEZA MKWARA MZITO

AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wachezaji wote wapo tayari kwa msimu mpya wa 2023/24.

Simba ilipashana na mataji msimu wa 2022/23 ambapo ni Yanga walitwaa mataji yote kuanzia Ngao ya Jamii, Kombe la Azam Sports Federation.

Katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Yanga iliwatungua mabao 2-1 Simba kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa na mtupiaji wa mabao ya Yanga ni Fiston Mayele.

Mayele hatakuwa ndani ya Yanga baada ya kupata changamoto mpya msimu wa2023/24 atakuwa ndani ya Pyramids ya Misri.

Mastaa wa Simba ikiwa ni pamoja na Luis Miquissone, Clatous Chama, Fabrice Ngoma, Kibu Dennis, John Bocco wameweka kambi Uturuki ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya.

Ni Agosti Mosi msafara wa kikosi cha Simba unatarajiwa kuwasili Bongo baada ya kambi ya muda iliyoanza Julai 12 huku wakiwa wanaelekea kwenye Simba Day, Agosti 6.

Ally amesema kuwa wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya msimu mpya na watatoa burudani kubwa kila mchezo.

“Wachezaji wa mpira wote wapo fiti kwa msimu mpya na juhudi wanazoonyesha kwenye maandalizi ni picha kubwa kuelekea kwenye ushindani mpya ndani ya msimu mpya.

“Ukianza na Luis, Kibe Dennis, Ngoma, Chama hawa wote wanafanya vitu vikubwa na vizuri kwenye mazoezi hilo linatupa nguvu ya kuamini kwamba tunakwenda kwenye ushindani mkubwa tukiwa na wachezaji imara.

“Kwa msimu mpya tunakwenda kuanza kwa mtindo mpya wa kusaka ushindi kila mechi huku tukiwapa burudani mashabiki hilo linakwenda kudhihirika Simba Day kisha kwenye mechi zinazofuata,” amesema Ally.