TAYARI ile Droo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na ile ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa imeshafahamika.
Wawakilishi wetu kutoka Tanzania bara na visiwani wamewatambua wapinzani wao ambao watakutana nao kwenye mechi za ushindani.
Yanga wanakumbuka rekodi yao bora ya kutinga fainali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na sasa kibarua kingine kimeanza kwao.
Singida Fountain Gate ni msimu wao wa kwanza kwenye anga la kimataifa lakini wana wachezaji ambao wameshawahi kucheza katika hatua hizo.
Yanga wana kazi ya kuendelea pale walipoishia huku Simba wao wakigotea hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Singida Fountain Gate na Azam FC kwenye Kombe la Shirikisho Afrika wana kazi ya kufanya kwenye mechi zote ili kufikia malengo.
Kwa timu ambazo zinatoka bara na visiwani ni muda wa kufanya kweli kwenye anga la kimataifa ili kuwapa furaha mashabiki na kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.
Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni Simba na Yanga wakati zile ambazo zitakwenda kucheza Kombe la Shirikisho ni Singida Fountain Gate na Azam FC hizi ni kutoka bara.
Yanga wao wataanzia hatua ya awali wakati Simba wao wakianza ile hatua ya pili jambo ambalo Yanga wamefahamu kuwa watakwenda kucheza na ASAS Djibout wakati Azam wao watakwenda kucheza na Bahir City ya Ethiopia wakati Singida wakitarajia kucheza na JKU ya Zanzibar.
Simba wao watasubiri mzunguko wa awali umalizike kisha mzunguko wa pili wanatarajiwa kucheza na mshindi kati ya Afrika Stars ya Namibia dhidi ya Power Dynamo ambao ni mabingwa kwenye ligi ya Zambia.
Hivyo kikubwa ni kwa timu zetu zijipange mapema ili kuhakikisha kuwa zinakwenda kufanya vizuri katika mashindano haya,litakuwa ni jambo jema kwa timu zetu zote kutoka bara na visiwani zikipata matokeo chanya.
Yaani wale ammbao watashiriki kombe la shirikisho waende hatua ya makundi na wale ambao wanakwenda Ligi ya Mabingwa Afrika wote waende katika hatua ya makundi hakika mtakuwa mmeliheshimisha taifa letu na ligi yetu kwa ujumla.
Kila kitu kinawezekana kikubwa ni mipango kwa sasa na kwa kuwa wapinzani wameshajulikana ni muda wa wa kupanga mipango makini itakayokuwa na majibu wakati ujao.