SINGIDA FOUNTAIN GATE KUWATAMBULISHA NYOTA WAPYA

IMEELEZWA kuwa nyota watatu wanatarajiwa kutambulishwa siku ya Singida Fountain Gate ikiwa ni zawadi yao kwa mashabiki msimu wa 2023/24.

Taarifa zimeeleza kuwa Singida Fountain Gate ambayo imewatambulisha baadhi ya nyota wao ikiwa ni Yahya Mbegu huku ikiwaongezea mikataba Bruno Gomes, Aziz Andambwile bado haijamaliza kusajili.

“Kuna wachezaji watatu ambao hawajatajwa popote kwa sasa hao watatambulishwa siku ya Singida Fountain Gate na itakuwa ni zawadi kwa mashabiki wa timu,” ilieleza taarifa hiyo.

Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Masanza amesema kuwa maandalizi ya Singida Fountain Gate yanakwenda vizuri.

“Maandalizi yanakwenda vizuri na kutakuwa na mambo matano ambayo yatafanyika ikiwa ni pamoja na utambulisho wa wachezaji na benchi la ufundi kwa msimu mpya wa 2023/24.

“Pia kutakuwa na mechi za kirafiki kwa timu ya Wanawake na ile ya Wanaume hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia burudani,” amesema Masanza.

Timu hiyo ipo chini ya Kocha Mkuu, Hans Pluijm ambaye anaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu wa 2023/24.