SINGIDA FOUNTAIN GATE YAPANIA KUFANYA KWELI

UONGOZI wa Singida Fountain Gate umeweka wazi kuwa utafanya kwenye anga la kitaifa na kimataifa kutokana na mipango makini iliyopo ndani ya timu hiyo inayodhamiwaniwa na SportPesa Tanzania.

Singida Fountain Gate ni miongoni mwa timu zitakazoiwakilisha Tanzania kwenye mechi za kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza ligi ikiwa nafasi ya nne.

Singida Fountain Gate imeweka kambi Arusha kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2023/24 unaotarajiwa kuanza Agosti.

Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Massanza amesema kuwa wanatambua ushiriki wao kwenye mechi za kimataifa ni muhimu kufanya maandalizi mazuri.

“Tunahitaji kufanya kweli kwenye mechi zetu za kitaifa na kimataifa ndio maana hata usajili wetu ni ule unaozingatia maboresho kwenye kikosi chetu.

“Wale waliopo wanatambua kwamba kazi itakuwa kubwa na ambao wanakuja wengi wanatambua wana kazi ya kufanya ili kuendeleza ubora na ushindani kwenye mechi zetu,” amesema Masanza.

Miongoni mwa wachezaji ambao wameanza mazoezi ndani ya Singida Fountain Gate ni pamoja na Deus Kaseke, Yahya Mbegu.