SABABU ZA KOCHA MPYA KMC ZATAJWA

UONGOZI wa KMC umebainisha kuwa ujana ni moja ya sababu zilizompa kazi Abdi Hamid Moallini ambaye ametambulishwa kuwa kocha mpya wa KMC rasmi Julai 12 2023.

Mstahiki Meya ya Kinondoni, Songoro Mnyonge Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KMC amesema kuwa miongoni mwa vigezo vilivyowafanya wakamchagua kocha huyo ni pamoja na ujana.

KMC ni mashuhuda wa Yanga ikitwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2022/23 na pia ni mashuhuda Singida Big Stars ikiwa ndani ya nne bora.

Ikumbukwe kwamba Singida Big Stars ni msimu wake wa kwanza ndani ya ligi na itashiriki kwenye mashindano ya kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Mnyonge amesema:” Miongoni mwa sifa ambazo zimetufanya tukampa kazi kocha huyu ni pamoja na ujana kwani anajukumu la kuwaongoza vijana wenzake na watakuwa wanaelewana.

“Pia ni weledi kwenye soka kwani kazi zinaonekana na anajua mpira hata umri pia hilo tumezingatia pamoja na uzoefu wake kwenye soka.

“Ukiangalia kwenye CV amewahi kuifundisha Azam FC na alifanya kazi nzuri tukaona badala ya yeye kurejea Azam FC tukaona ni bora yeye aje hapa kwani Azam FC tayari imeshapata kocha,” .

Kocha huyo amesema: “Nafasi nyingine kwangu kuwa ndani ya KMC ni muda mzuri na ninatambua kwamba hii timu ina wachezaji wazuri hivyo tutapambana kufanya kazi nzuri na ninatambua ligi ni ngumu,”.