IPO wazi kuwa kila timu kwa sasa ipo chimbo ikifanya kazi kubwa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2023/24.
Tunaona Azam FC wapo tayari wapo kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya na kazi yao ya kwanza itakuwa kwenye nusu fainali Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Simba nao wapo kambini na mchezo wao wa kwanza utakuwa dhidi ya Singida Fountain Gate mchezo wa nusu fainali Ngao ya Jamii pale Tanga.
Kila timu inapambana kufanya kazi kubwa ambapo tunaona usajili kwa timu zote unaendelea huku nyingine zikivutia kasi.
Namungo ipia imeshamalizana na Erasto Nyoni hivyo ipo tayari kwa ajili ya msimu mpya kufanya maboresho zaidi.
Majigambo yanayofanyika kwa sasa majibu yake yanakuja kwa sababu muda huwa hauna tabia ya kusubiri unatoa majibu yake bila kuchelewa.
Kwenye usajili ambao unafanyika ile ripoti ya benchi la ufundi iliyotolewa ni muhimu itumike kwa umakini kwa kuwa hakuna kiongozi atakayepanga kikosi cha ushindi.
Benchi la ufundi linatambua nani atakuwa kwenye eneo lipi na wakati gani hiyo inaongeza nguvu ya ushindani na kumpa uhuru mwalimu kuchagua aina ya kikosi anachohitaji.
Kikosi cha ushindi kinatengenezwa na mwalimu mwenyewe kutokana na aina ya timu ambayo anakwenda kukutana nayo hivyo muda ni sasa kufanya yote kwa ajili ya msimu ujao.
Ushindi unahitajika na hautokei kwa bahati mbaya bali ni mipango makini wakati huu wa maandalizi ikiwa ni pamoja na kufanya usajili makini.
Wachezaji ambao watapata nafasi kuanza changamoto mpya katika timu nyingine jukumu lao ni moja kufanya kazi kweli bila kuogopa.
Bahati ambayo wamekutana nayo kupata timu mpya ni muhimu kuitumia kwa umakini kwani wapo wengine wenye uwezo mkubwa zaidi yao lakini hawajapata nafasi kwenye timu mpya, hivyo tu basi.
Matokeo mazuri watakayoonyesha uwanjani itakuwa ni malipo ya madeni ambayo wameyaacha kwa mashabiki hivyo watakuwa wametimiza wajibu wao na kuwapa furaha mashabiki na viongozi pia.