SIMBA:BADO MASHINE NYINGINE ZINAKUJA

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa wapinzani wao hawataamini macho yao kwa msimu mpya wa 2023/24 kutokana maandalizi wanayofanya.

Roberto Oliveira amepewa jukumu la kuinoa timu hiyo iliyopishana na mataji yote msimu wa 2022/23 kuanzia Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Mapinduzi, Azam Sports Federation na Ligi Kuu Bara yaliyokwenda Yanga.

Maandalizi yao kwa msimu wa 2023/24 yameanza na kambi inatarajiwa kuwa Uturuki ambapo wameanza safari Julai 11 kuelekea Uturuki na mchezo wao wa ufunguzi itakuwa dhidi ya Singida Fountain Gate kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Mkwakwani, Tanga.

Ahmed Ally Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wapinzani wao hawataamini macho yao kutokana na mipango makini waliyonayo.

“Hakika ni furaha kubwa itakuwa kwa mashabiki wa Simba, tumekuwa wanyonge msimu wa 2022/23 kwa kukwama kufanikisha malengo yetu sasa wapinzani wetu hawataamini macho yao.

“Ni mipango makini inasukwa kwenye kila idara kuanzia benchi la ufundi mpaka wachezaji wenyewe ni mwendo wa kutoa furaha kwa mashabiki na kutimiza majukumu yao, wachezaji waliopo ndani ya kikosi wote ni bora.

“Mashabiki wasikate tamaa wasichoke kutuombea dua na kuendeleza ushirikiano kama sera yetu inavyosema Simba nguvu moja,” amesema Ally.