MAPENDEKEZO BENCHI LA UFUNDI YAFUATWE KUEPUKA LAWAMA

HEKAHEKA za usajili kuelekea msimu mpya wa mashindano kwenye Ligi Kuu Bara zimeanza baada ya msimu wa mashindano wa 2022/23 kumalizika.

Ipo wazi kuwa Yanga wamefanikiwa kubeba kila kombe kwenye mashindano ya ndani kuanzia Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na lile taji la Kombe la Shirikisho la Azam.

Timu zote iwe zile zinazoshiriki Ligi ya Wanawake, Championship muhimu kufanya kazi kubwa kwenye usajili.

Singida Fountain Gate, Namungo, Geita Gold, Azam FC mpaka KMC ni muda wa kufanya usajili ulingana na mahitaji ya benchi la ufundi.

Kipindi hiki timu zinapaswa kuwa makini katika kuhakikisha wachezaji ambao watasajiliwa wanaendana na mahitaji ya benchi la ufundi na usiwe usajili wa kukurupuka au wa kuwafurahisha mashabiki.

 Ni kipindi ambacho kila kiongozi au mtu mwenye ushawishi ndani ya timu atakuja na jina la mchezaji wake mezani na kulazimisha asajiliwe pasi na kuangalia kama mchezaji huyo ana tija ndani ya kikosi au la.

Kuna kasumba ambayo imekuwa ikiendelea kwenye ligi yetu hususan kwenye timu kubwa na zile za madaraja ya kati ambazo zinakuwa na bajeti kubwa kuelekea kipindi cha usajili ambapo usajili umekuwa ukifanyika kiholela bila kuzingatia mahitaji ya benchi la ufundi.

Jambo la kusikitisha ni pale mambo yanapogeuka makocha wamekuwa wakibebeshwa zigo la lawama ambalo hawakustahili hata kidogo, hivi karibuni tumeona timu kadhaa zikiingia hasara ya kusajili wachezaji kwa fedha kubwa ambao wameshindwa kuonyesha chochote uwanjani na mwisho wa siku mikataba yao imevunjwa huku timu zikipata hasara kubwa.

Ni lazima uwepo utaratibu wa kufanyika kwa tathmini ya kina kabla ya usajili wa wachezaji kufanyika, ni lazima timu zijiwekee vigezo (standards) ambazo mchezaji anapaswa kuzifikia ili aweze kusajiliwa na timu husika kwa mfano mchezaji lazima awe kwenye timu ya taifa kwa wachezaji wa kigeni ili kuondoa lundo la wachezaji mizigo ndani ya timu.

Ni wazi makocha watakuwa wameandaa ripoti zao kuelekea msimu mpya wa mashindano kuona ni mchezaji gani anahitajika ndani ya kikosi na nani hahitajiki kikosini na si viongozi kuingilia mipango ya benchi la ufundi na kujikuta wanasajili wachezaji kwa mapendekezo yao wenyewe.

Siyo muda wa kiongozi kuonyesha ufahari wake katika kufanya usajili ambao ni kinyume na matakwa ya benchi la ufundi kwa ajili ya kutafuta umaarufu kwa mashabiki ambao hauna tija yoyote na baadaye mambo yanapokuwa magumu makocha wanamekuwa wakiadhibiwa kwa uzembe wa watu wachache.

Usajili wa mihemko hiki siyo kipindi chake, bali jikiteni katika kufanya sajili ambazo zitafanya vikosi vyenu kuwa tishio na si kutafuta visingizio hapo baadae baada ya kufeli kwenye mipango yenu.

Kuna timu kadhaa tumeona zimefanya usajili wa mihemko na mwisho wa siku wanajikita kwenye visingizio ambavyo havina msingi baada ya wachezaji wao kufeli.

 Msijikite kwenye  kufanya usajili wa kukomoana, kuona mchezaji anatakiwa na timu fulani na nyie mkajikuta mnaingilia kati dili hilo licha ya kuwa mchezaji hayupo kwenye mipango yenu, usajili uzingatie mahitaji ya benchi la ufundi kwa ustawi wa timu zenu. Kila la heri.

ReplyForward