ALLY Kamwe Ofisa Habari wa Yanga amesema wamepata mualiko maalumu kutoka Malawi jambo ambalo ni heshima na wanalichukua kwa mikono miwili.
Kamwe ameweka wazi kuwa watacheza mchezo maalumu kwenye maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru wa Malawi Julai 6, 2023 ikiwa ni mualiko maalumu kutoka Malawi hivyo Yanga watakuwepo huko.
Kamwe amesema:”Ni heshima kubwa sana kwa klabu yetu na kwa Taifa kwa ujumla kupata mualiko huu na tuna amini kwamba tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu maalumu.
“Mgeni wa heshima kwenye sikukuu za uhuru wa Malawi ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Malawi ikatupa heshima hii ya kipekee kwa mualiko huu mkubwa na wa kihistoria.
“Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa wachezaji wetu ambao watatoka mapumzikoni na kuungana nasi kwenda kuiwakilisha nchi na klabu yetu kwenye mualiko huu mkubwa.
“Tunatarajia kuondoka siku ya Jumatano na kama kawaida yetu ndege maalum kabisa itatupeleka Malawi na kutusubiri kisha tutarejea Dar siku ya Alhamisi baada ya sherehe hizo,” amesema.