SINGIDA FOUNTAIN GATE WAPEWA M 50 NA SportPesa

KAMPUNI ya kubashiri ya SportPesa leo Juni 3 imekabidhi hundi ya shilingi milioni 50 kwa Klabu ya Singida Fountain Gate FC ambayo zamani ilikuwa inaitwa Singida Big Stars.

Hiyo yote ni baada ya kukamilisha msimu ikiwa nafasi ya nne katika NBC Premier League msimu wa 2022/23.

Katika hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya kampuni hiyo Masaki, Dar na waliohudhuria kutoka SportPesa ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Tarimba Abbas, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Sabrina Msuya, kutoka Singida Fountain Gate FC ni Makamu wa Rais utawala na fedha John Kadutu, Mkurugenzi wa Masoko Tabitha Kidawadawa.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi SportPesa Tarimba Abbas ameweka wazi kuwa kazi kubwa imefanywa na wachezaji kupambana jambo ambalo wanastahili pongezi.

“Ninapenda kuwapongeza wachezaji na viongozi wa Singida Fountain Gate FC kwa hatua waliopiga katika msimu huu uliokwisha kwa kuonyesha ni kwa jinsi gani walidhamiria kupata mafanikio au kufika mbali kisoka.

“Napenda kuwapongeza viongozi na wachezaji wa Singida Fountain Gate FC kwa mafanikio ambayo mmeyapata, kwani mmewapa heshima kubwa wana Singida kwa ujumla wao popote pale walipo.

“Kubwa zaidi ni heshima mliyotupa sisi wadhamini wenu wakuu kwa namna mlivyoweza kupigania chapa yetu kwa namna ambavyo mlijipambanua uwanjani, kama washindani wa kweli na si washiriki.

“Nafasi hii ya nne mliyoishika ni fursa kwa timu yenu kucheza vizuri zaidi kwenye msimu mpya unaokuja, na pia ni ishara nzuri kwani mnaweza kupambana na kupanda nafasi mbili za juu na pengine hata kuchukua ubingwa.

“Nachukua pia fursa hii, kuwapongeza kwa kufanikiwa kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, ya kombe la Shirikisho barani Afrika, msimu unaoanzia 2023/2024,” amesema.

 Makamu mwenyekiti John Kadutu alianza kwa kusema:“Nichukue nafasi hii kuipongeza SportPesa kwa kufuata kila kipengele cha makubaliano yaliyopo kwenye mkataba huu kwa kutoa bonus ya Sh. 50,000,000 kama timu itaingia tano bora katika ligi ya msimu husika.

“Kwa kipindi cha miaka 4 toka msimu wa mwaka 2022/2023. Jambo hili limekuwa na tija hivyo kuamsha morali ya wachezaji na watendaji katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika kuipigania klabu kufanya vizuri.

“Nichukue nafasi hii kwa mara nyingine kuwashukuru SportPesa kwa kutujali na kuwa karibu na timu yetu pale ambapo tunahitaji msaada wenu’, ” asema John.