YANGA WANA JAMBO KUBWA LA MTIKISIKO

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa unakuja mtikisiko kwenye suala la usajili kutokana na mipango makini waliyonayo.

Chini ya Kocha Mkuu Nasreddine Nabi msimu wa 2022/23 Yanga ilikomba mataji yote ya ndani ikiwa ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Azam Sports Federation.

Katika anga la kimataifa Yanga safari yao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika imegotea nafasi ya pili ikiwa ni rekodi kubwa iliyoandikwa na Nabi ambaye hatakuwa na timu hiyo msimu wa 2023/24.

Ni Miguel Gamondi raia wa Argentina atakuwa akikikonoa kikosi cha Yanga baada ya kukabidhiwa mikoba ya Nabi.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema kuwa kwenye eneo la kuboresha kikosi hawatanii kwani hilo lipo na lazima litafanyika.

“Katika eneo ambalo hatutanii ni kwenye maboresho ya kikosi na tunaamini kwamba mtikisiko unakuja na wachezaji wazuri watakuwa ndani ya timu.

“Kila kitu kwa utaratibu wake na tunaamini tutafanikiwa hivyo hakuna sababu ya kuwa na hofu kwa mashabiki muda utazungumza,” .