>

FISTON MAYELE BALAA LAKE LIPO HAPA

MZEE wa kutetema Fiston Mayele wa Yanga mguu, ‘guu’ lake la kulia lina balaa kitaifa na kimataifa kwenye kutupia mabao kutokana na kufunga mabao mengi kwenye mechi za ushindani.

Nyota huyo wa Yanga ana tuzo ya mfungaji bora kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa ametupia jumla ya mabao 7 na kuvaa medali ya mshindi wa pili Afrika.

Mbali na hayo mabao 7 pia kwenye ligi ni namba moja kwa mastaa wenye mabao mengi akiwa ametupia mabao 16 hivyo kwenye mashindano hayo makubwa mawili katupia jumla ya mabao 23.

Katika anga za kimataifa Mayele katupia mabao sita akitumia mguu wa kulia na mguu wa kushoto katupia bao moja ambapo aliwafunga Real Bamako ugenini ila Uwanja wa Mkapa aliwatungua kwa kutumia mguu wa kulia ikiwa ni timu iliyofungwa na Mayele nje ndani kwa miguu yote miwili.

Nyingine ambazo kazitungua Mayele ni US Monastri bao moja, Rivers United mabao mawili, Marumo Gallants bao moja na USM Alger bao moja kwenye fainali ya kwanza Uwanja wa Mkapa.

Kwenye ligi katika mabao 16 aliyofunga ndani ya Yanga ni mabao 12 katumia mguu wa kulia na mabao mawili kwa pigo la kichwa huku akitumia mguu wa kushoto kufunga mabao mawili.

Jumla Mayele katumia mguu wa kulia kufunga mabao 18 ule wa kushoto mabao matatu na katumia kichwa kufunga mabao mawili.