KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Mbwana Makata amesema kuwa miongoni mwa sababu ambazo zimefanya timu hiyo kushindwa kubaki ndani ya ligi ni pamoja na suala la usajili na ubora wa wachezaji.
Mei 12 ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Simba na kuifanya iwe timu ya kwanza kushuka daraja, msimu ujao itashiriki Championship.
Imegotea nafasi ya 16 ikiwa na pointi 20 Simba ipo nafasi ya pili na pointi 67 mabingwa ni Yanga wenye pointi 74 baada ya kucheza mechi 28.
Tayari Yanga wametangazwa mabingwa baada ya ushindi wa mabao 4-2 Dodoma Jiji, mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Makata amesema kuwa walikuwa wanajituma kutafuta matokeo kwenye mechi ambazo wamecheza lakini matokeo yalikuwa tofauti na walivyotarajia.
“Tulikuwa tunahitaji kupata ushindi lakini tulishindwa na kuna sababu nyingi ikiwa ni pamoja na usajili kwani ligi hii ina ushindani mkubwa inahitaji wachezaji imara watakaokuwa na uwezo wa kushindana.
“Kwa mfano mchezo wetu dhidi ya Simba hatujashindwa kutokana na mbinu bali wachezaji wa Simba wao walikuwa bora zaidi yetu lakini tuna kazi kufanya kwa ajili ya mechi zilizobaki.
“Kilichobaki kwa sasa kuangalia mechi zilizobaki na changamoto hazikimbiwi tutakuwa pamoja ili kujifunza kwenye mapito yote,” .