WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga za kimataifa Simba mbio zao zimegote hatua ya robo fainali baada ya kufungashiwa virago na mabingwa watetezi Wydad Casablanca.
Wakati yakitokea kwa Simba kufungashiwa virago watani zao wa jadi Yanga wametinga hatua ya nusu fainali dhidi ya Rivers United kutoka Nigeria.
Hakika moja ya mechi mbili zilizokuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote Simba na Yanga na nafasi ilikuwa wazi kwa kila timu kutinga hatua ya nusu fainali.
Tumeona Yanga walitumia vema mechi ya ugenini kumaliza mchezo kisha nyumbani wakakamilisha hesabu Simba ngoma ilikuwa ngumu kila pande mchezo wa nyumbani walishinda wakashindwa kutumia nafasi na mchezo wa ugenini wakafungwa wakashindwa kutumia nafasi.
Mwisho ni Wydad wamekamilisha safari kwa kuondoa Simba kwa ushindi wa jumla ya penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1.
Hii ni hadithi ambayo imekuwa na mwendelezo wa muda mrefu hasa inapofika hatua ya Simba kuvunja mwiko wao kwenye anga za kimataifa.
Robo fainali imekuwa ni mafanikio ya Simba kwa hili wanapaswa kupongezwa lakini ni muhimu kujifunza kwa yale ambayo yamepita.
Mwendo mzuri mwanzo mwisho wanagotea palepale hii ni somo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi kwa kufanya tathimini kwa kina wapi ambapo wamekuwa wakikosea.
Kwenye upande wa kumaliza mechi Uwanja wa Mkapa hatua ya robo fainali bado kazi imekuwa namna ileile hata walipokuwa kwenye hatua ya Kombe la Shirikisho waligotea hapo.
Wakiwa wanapewa nafasi ya kutinga nusu fainali wanaondolewa kwa changamoto za penalti ina maana kwamba bado yale makosa ya wakati uliopita hayajafanyiwa kazi.
Basi ni muda mwingine sasa kufanya uchanganuzi wa kina na kuweka malengo makubwa kwa kuwa nafasi na uwezo wanao wakati ujao hadithi ya robo fainali iwekwe kando safari iwe mpaka fainali.