NAMNA KAZI ILIVYOGOTA MWISHO KWA SIMBA MBELE YA WAARABU

KAZI ya wawakilishi wa Tanzania Simba kwenye hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika imegotea mwisho dhidi ya Wydad Casablanca hatua ya roo fainali baada ya kuondolewa kwa jumla ya penalti 4-3.

Matokeo ya jumla ni Wydad 1-1 Simba kwa kuwa kila timu ilishinda bao moja kwenye uwanja wa nyumbani hivyo Simba wanakazi ya kujipanga wakati ujao kumaliza mechi nyumbani mapema.

Wanaobaki kwenye mashindano ya kimataifa kwa sasa ni Yanga ambao wapo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika nao wakiwa hatua ya robo fainali kete yao ijayo ni dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Yanga inafaida ya mabao 2-0 ambayo walipata ugenini hivyo ina kazi ya kulinda ushindi na kuongeza mabao mengine ikiwa watafungwa Uwanja wa Mkapa nao mwendo utagotea mwisho.

Katika mchezo wa jana Dakika 15 za mwanzo Simba walicheza kwa utulivu mkubwa na nidhamu wakiwa na mpira lakini mbinu ziligotea dakika ya 22.

Bao la kwanza lilipachikwa na nyota Junior Boll dakika ya 23 kwa pigo huru la kichwa akiwa mbele ya mabeki wa Simba ambao walikwama kuoka hatari hiyo na lilidumu mpaka dakika ya 90.

Licha ya kufunga bao hilo bado Simba walionyesha uimara kwenye kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Shukrani kwa kipa namba mbili wa Simba, Ally Salim ambaye alikuwa imara kwa kuokoa hatari ikiwa ni pamoja na dakika ya 13,15,16,32,40,42.

Kiungo Clatous Chama alikuwa wa kwanza kuonyeshwa kadi ya njano kwenye mchezo ikiwa ni dakika ya 7 na alifanya jaribio dakika ya 44 ambalo halikulenga lango.

Jean Baleke alikuwa chini ya ulinzi mkali wa mabeki wa Wydad ambao walikuwa wakienda naye hatua kwa hatua ndani ya Uwanja wa Mohamed V.

Ni nyota wawili walikwama kufunga penalti kwa Simba, Shomari Kapombe na Clatous Chama hivyo mwendo wa Simba umegota mwisho mpaka wakati ujao.