KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira amesema kuwa anafurahishwa na ushirikiano uliopo kwenye safu ya ulinzi kwenye mechi ambazo wanacheza kitaifa na kimataifa.
Simba imetoka kupata ushindi dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa na ilipata ushindi mchezo wake uliofuata dhidi ya Wydad Casablanca ambao ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hiyo kwenye anga za kimataifa katika hatua ya makundi baada ya kucheza mechi sita ilitunguliwa mabao 7 katika robo fainali ya kwanza haikufungwa.
Kituo kinachofuata ni dhidi ya Wydad Casablanca mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mohamed V Aprili 28, saa 10:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Oliveira amesema kuwa mpira ni mchezo wa makosa na wachezaji wamekuwa wakiimarika kila baada ya mchezo.
“Unaona kwenye upande wa ulinzi ninafurahishwa na namna wanavofanya kazi mtazame Mohamed Hussein, (Zimbwe Jr), Kapombe, (Shomari), Inonga, (Henock) kila mmoja anafanya kazi kwa kujituma.
“Wote wanashirikiana na hii inaongeza nguvu kwenye eneo hilo kwani ili ushinde ni lazima uhakikishe kwamba haufungwi hili ni jambo la msingi na tunalifanyia kazi kila wakati,” alisema Oliveira.
Inonga ambaye anafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na mshikaji wake Joash Onyango jina lake limepenya kwenye kikosi bora cha CAF cha wiki mchezo wa robo fainali ya kwanza.