MWAMBA WA LUSAKA ANAJITAFUTA

CLATOUS Chama ni namba moja kwenye kutengeneza pasi za mwisho kwenye ligi akiwa nazo 14 kibindoni na ametupia mabao matatu kwenye nyavu za wapinzani bado anajitafuta kwa sasa.

Kwenye msimamo Simba ipo nafasi ya pili na vinara ni watani zao wa jadi Yanga.

Ngoma ni nzito kwenye kufunga na kutoa pasi za mwisho kwenye mzunguko wa pili kwa kuwa kapitisha mechi kadhaa bila kufunga wala kutoa pasi ya bao.

Wakati Simba ikishuhudia ubao wa Uwanja wa Manungu ukisoma Mtibwa Sugar 0-3 Simba mabao yote alifunga Jean Baleke huku pasi zikitolewa na Saidi Ntibanzokiza, Moses Phiri na Shomari Kapombe lakini mwamba hakutoa pasi iliyoleta bao licha ya kukiwasha kwenye mchezo huo.

Mara ya mwisho Chama kufunga kwenye ligi ilikuwa ni Desemba 18,2022 dhidi ya Geita Gold,Uwanja wa CCM Kirumba na pasi ya mwisho alitoa Uwanja wa Mkapa Februari 3 dhidi ya Singida Big Stars.

Alikuwa kikosi cha kwanza Aprili 16 ubao wa Uwanja wa Mkapa uliposoma Simba 2-0 Yanga alionyesha makeke yake lakini jitihada zake ziligonga mwama kutokana na wale aliowatengeneza pasi kukwama kufunga.

Raia huyo wa Zambia amehusika kwenye mabao 17 kati ya 62 ambayo yamefungwa na timu hiyo kwenye ligi baada ya kucheza mechi 26 ni chaguo la kwanza la Kocha Mku, Roberto Oliveira hivyo bado anajitafuta.