BALEKE, MAYELE WAINGIA KWENYE VITA HII NGUMU

MITAMBO ya mabao kwenye timu zenye ngome pale Kariakoo, Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira na Yanga inayonolewa na Nasreddine Nabi wameingia kwenye vita nyingine kimataifa.

Ni ile ya kupambania timu zao kutinga hatua ya nusu fainali kwenye mashindano ya kimataifa ambayo wanashiriki kwa kukamilisha dakika 90 za ushindi kwenye mechi za robo fainali.

Baleke alianzisha mwendo kwenye mchezo dhidi ya Wydad Casablanca kwa kufunga bao la ushindi hatua ya robo fainali dakika ya 30, Uwanja wa Mkapa akitumia pasi ya Kibu Dennis.

Kibarua cha pili ni kushirikiana na wachezaji wenzake kukamilisha ngwe ya pili ugenini Uwanja wa Mohamed V kulinda ushindi huo ama kushindi ili watinge hatua ya nusu fainali.

Mayele ambaye alikuwa na kazi kubwa kwenye Karikaoo Dabi alipokuwa chini ya ulinzi wa Mzamiru Yassin yeye alianzisha mwendo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United ugenini kwa kufunga mabao mawili dakika ya 71 na 82 akitumia pasi za mzawa Bakari Mwamnyeto.

Vita yake ni kukamilisha hesabu kwenye mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa ambao mshindi wa jumla atakata tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali.

Mbali na vita hiyo, washambuliaji hao kila mmoja anapambania kuongeza idadi ya mabao ambapo Mayele kafikisha mabao 50 akiwa na Yanga kwenye Kombe la Shirikisho ana mabao matano huku Baleke akifikisha jumla ya mabao 15, kwenye ligi ya mabingwa mabao manne.