AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na MawasilianoSimba amesema wataushangaza ulimwengu kwa kuwapelekea moto wapinzani wao Wydad Casablanca kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira inatarajiwa kusaka ushindi kwenye mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ally amesema kuwa wamekuwa na muda mzuri kufanya maandalizi kwa mchezo huo jambo litakalowashangaza wengi kutokana na matokeo watakayopata.
“Tunakwenda kuwashangaza Wydad kwa kile ambacho watakiona kwa kuwa hawataamini macho yao hata ulimwengu wa mpira nao utapata kitu ambacho kitawashangaza kutokana na imani yao.
“Wengi walituondoa kwenye reli na kuamini kwamba mwendo tumeumaliza baada ya kupangwa na vigogo Wydad, hakika tunakwenda kufanya jambo la kipekee na wachezaji wapo tayari kuona tunapata ushindi.
“Roho ambayo wataivaa kwenye mchezo wetu ni ile ya Simba mwenyewe na tunaamini watajituma na kucheza kwa tahadhari kubwa, mashabiki wajitokeze kwa wingi,” amesema Ally.
Leo Aprili 22, Simba inatarajia kucheza mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Wydad Uwanja wa Mkapa.Ikumbukwe kwamba Wydad ni mabingwa watetezi.