LICHA ya kazi kubwa ambayo aliifanya Mzamiru Yassin kwenye Kariakoo Dabi kuna faulo za hatari alizicheza mtindo wa nge kwa nyota Fiston Mayele.
Hakika Mayele kuna wakati aliomba poo na alikasirika kwelikweli kutokana na kuchezewa faulo na kiungo Mzamiru.
Ile iliyompa maumivu makubwa ilichezwa dakika ya 46 na Mzamiru wakati akiokoa hatari kuelekea kwenye lango la Ally Salim kipa namba tatu wa Simba.
Kukata umeme kwa Mzamiru hakuna tatizo ni sawa kwa kuwa anatimiza majukumu yake lakini ni muhimu kuzingatia afya ya wapinzani.
Mpira sio vita bali hesabu za kusaka ushindi kwa kutumia makosa ya mpinzani ndani ya uwanja baada ya dakika 90 maisha yanaendelea.
Ilikuwa hivyo vita ya Sadio Kanoute na Khalid Aucho kwenye moja ya mchezo wa watani na Kanoute alikwama kueyusha dakika 90 kutokana na kupata maumivu hii sio sawa kwa wachezaji ambao wana uwezo mkubwa na wanacheza mechi za kimataifa.
Ikumbukwe kwamba mchezaji hapendi kumuumiza mchezaji mwenzake hasa ukizingatia kwamba mpira wa miguu purukushani hazikosekani ni muhimu tahadhari kuchukua kwa kila mmoja.
Mayele alivumilia kwenye mchezo dhidi ya Simba na alipodondoshwa chini aliwaka kwa kuwa damu ilikuwa imechemka isingekuwa juhudi za wachezaji wengine kumzuia huenda angeambulia kadi.
Na ingekuwa ni kadi yake ya kwanza kwenye maisha ya soka kuipata kwenye ardhi ya Tanzania kwa kuwa tangu alipowasili Bongo hajaambulia kadi ya njano wala nyekundu.
Muhimu wachezaji kucheza kwa umakini bila kuhatarisha afya za wachezaji wa timu pinzani, mikato ya kimyakimya haipendezi.