KINZUMBI AIWAHI KAMBI YANGA

WINGA wa TP Mazembe ya DR Congo, Phillipe Kinzumbi, mwishoni mwa mwezi huu anatarajiwa kutua nchini tayari kwa kuingia kambini Yanga.

Nyota huyo ni kati ya wachezaji walio katika mipango ya kusajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao ambapo wikiendi iliyopita alipewa mkataba wa awali.

Usajili wa Kinzumbi ni chaguo la Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi ambaye alipendekeza asajiliwe kutokana na kuhitaji kuimarisha eneo la ushambuliaji.

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, zinasema mabosi wa Yanga wamekamilisha dili la winga huyo, na ataingia kambini mapema kwa ajili ya kuzoeana na wachezaji wenzake na mazingira.

Mtoa taarifa huyo alisema kingine kitakachomuwahisha kambini ni timu yake ya TP Mazembe kutoshiriki mashindano yoyote kwa sasa mara baada ya kuondolewa katika shirikisho.

“Kinzumbi anatarajiwa kutua nchini sambamba na kujiunga na kambi ya timu mwishoni mwa mwezi huu mara baada ya mabosi kukamilisha dili lake haraka.

“Hivyo Kinzumbi atakuwa mchezaji mpya wa kwanza kusajiliwa na kujiunga na kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

“Hivyo winga huyo hatakuwa mgeni na wenzake pamoja na mazingira ya hapa nchini, kwani hadi ligi ikianza msimu ujao atakuwa amezoea mazingira yote ya timu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Hivi karibuni, Kinzumbi alikiri kumalizana na mabosi wa Yanga na kudai ni suala la muda kwake kujiunga na timu hiyo.

“Nimemalizana na Yanga kwa asilimia kubwa, na muda wowote nitajiunga na timu hiyo,” alisema winga huyo raia wa DR Congo