BALEKE HAKAMATIKI, AMKALISHA MUSONDA

USAJILI wa Simba kwa mshambuliaji Mkongomani, Jean Baleke umeonekana kuwa bora zaidi ya straika wa Yanga, Mzambia, Kennedy Musonda.

Hiyo imetokana na kasi na ubora wake wa kufunga mabao tangu Mkongomani huyo ajiunge na Simba katika usajili wa dirisha dogo kama ilivyo kwa Musonda.

Usajili wa Baleke ulikuwa ukibezwa kutokana na kujiunga na timu hiyo kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya DR Congo.

Musonda alikuwa akitabiriwa kufanya vizuri kutokana na Yanga kuvunja benki kumnunua mshambuliaji huyo mwenye kasi akiwa na mpira.

Baleke tangu atue Simba, amefanikiwa kufunga mabao matano katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports bao moja, huku kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga matatu.

Upo uwezekano mkubwa wa Simba kumsajili Baleke moja kwa moja kutokana na kasi hiyo ya kufunga mabao akiwa na muda mchache tangu ajiiunge na timu hiyo.

Mabosi wa Simba hawahitaji kumpa muda Baleke kujiridhisha juu ya ubora wake na zaidi wampe mkataba wa muda mrefu, kwani ya muda mfupi ametoa mchango mkubwa katika timu.

Usajili wa Baleke unaweza kuufananisha na usajili wa Musonda ambaye kwa sasa ana mabao mawili katika Kombe la Shirikisho Afrika, huku akiwa na mabao matatu Kombe la Shirikisho la Azam Sports, lakini Ligi Kuu Bara hana bao.