YANGA :TUNAHITAJI MAOMBI KIMATAIFA

IKIWA leo inatarajiwa kutupa kete yake ya tatu kimataifa dhidi ya Real Bamako mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika benchi la ufundi limeomba dua kutoka kwa Watanzania.

Yanga ipo nafasi ya pili kwenye kundi D baada ya kucheza mechi mbili imekusanya pointi tatu sawa na TP Mazembe wakiwa tofauti kwenye mabao ya kufunga na kufungana.

Mchezo uliopita Yanga ilishinda mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe uliochezwa Uwanja wa Mkapa kwa sasa kikosi kipo Mali kwenye maandalizi ya mwisho ya mchezo wao dhidi ya Real Bamako unaotarajiwa kuchezwa kesho.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze amesema kuwa wanatambua kazi kubwa ipo mbele yao dhidi ya Real Bamako wanachohitaji ni dua kutoka kwa Watanzania.

“Tunahitaji dua kutoka kwa Watanzania hasa ukizingatia tuna mchezo mgumu wanachopaswa ni kuendelea kutuombea nasi kwenye upande wa mbinu tunajipanga kufanya vizuri na inawezekana.

“Kwenye mechi hizi za kimataifa kila timu inahitaji ushindi na malengo yetu ni kuona tunafanikiwa kwenye kila hatua hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi tunaamini kazi itakuwa ngumu lakini tutafanya kazi kwa umakini,” amesema Kaze.