WINGA wa zamani wa Yanga na TP Mazembe, Chiko Ushindi Wakubanza, amesema kama Yanga watapambana zaidi na kucheza kwa moyo mmoja, basi watapata matokeo mazuri mbele ya TP Mazembe, huku akibainisha kwamba.
Ushindi ambaye aliitumikia Yanga msimu uliopita kwa mkopo akitokea TP Mazembe, kwa sasa anakipiga katika Klabu ya Don Bosco ya nchini DR Congo ambayo ipo chini ya TP Mazembe.
Akizungumza na Spoti Xtra, Ushindi alisema kama wachezaji wa Yanga watajituma na kucheza kwa umoja mkubwa, basi wanayo nafasi ya kupata matokeo ya ushindi mbele ya TP Mazembe, ambayo imekuwa ikipata shida ugenini katika siku za hivi karibuni tofauti na miaka ya nyuma.
“Yanga kama watapambana vizuri na TP Mazembe basi wanaweza kupata matokeo ya ushindi, ukiangalia Yanga kwa sasa wana kikosi kizuri ambacho kinaweza kupambana na kupata matokeo, ambacho wanatakiwa kukifanya Yanga kwa sasa ni kuhakikisha siku ya mchezo wanatakiwa kucheza kwa moyo mmoja, naamini watashinda.
“TP Mazembe ni timu nzuri, lakini kuna utofauti kidogo na miaka ya nyuma ambayo walikuwa wanaweza kwenda katika uwanja wowote kisha wakapata matokeo ya ushindi, lakini kwa sasa imekuwa tofauti kwani wamekuwa wakishinda zaidi nyumbani kuliko ugenini,” alisema mchezaji huyo.