KOCHA wa Simba, Mbrazil Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amefunguka kuwa, watakuja kuzifunga timu zote kwenye Uwanja wa Mkapa wakianza na Raja Casablanca kwa kuwa wachezaji wake muhimu akiwemo Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ watakuwa fiti.
Robertinho ameweka wazi kuwa, kilichowafanya wafungwe kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya wakiwa ugenini ni kukosa bahati kwa sababu kama kucheza wao waliucheza kuzidi wenyeji wao.
Kocha huyo mwenye mbwembwe nyingi alisisitiza kuwa baadhi ya wachezaji wake hawakuwa fiti kama Moses Phiri na Saido ambaye hakuwepo kabisa kwenye mchezo huo kwa sababu ya majeruhi.
“Mpango wetu wa sasa ni kushinda kila mechi tukiwa nyumbani, kuna wachezaji hawakuwa sawa kwenye mechi yetu ya kwanza. Hatukuwa na Saido kwenye kikosi pia. Bila shaka atakuwepo kwenye mechi na Raja.
“Wao ni timu kubwa, Simba pia ni timu kubwa na tumejipanga kushinda kwenye mech izote za nyumbani. Huo ndiyo mpango wetu kwa sasa,” alisema.
Simba baada ya mchezo wao na Horoya waliopoteza kwa bao 1-0, wanarejea nyumbani kucheza mchezo wa pili dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco Februari 18.