KOCHA Mkuu wa TP Mazembe mwenye uraia wa Ufaransa, Franck Dumas amesema kuwa ubora wa wachezji wa Yanga kama Aziz Ki na Fiston Mayele ni sababu ya wao kuwa siriazi ili kupata matokeo.
TP Mazembe wanatarajiwa kucheza na Yanga Jumapili katika Uwanja wa Mkapa ukiwa ndio mchezo wao wa kwanza ugenini mara baada ya kuanza nyumbani katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Real Bamako na kushinda 3-1 kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Akizungumza na Championi Jumatano, kocha huyo alisema kuwa, ubora wa wachezaji wa Yanga unasababisha mchezo wao kuwa mgumu ugenini na wanaamini kuwa watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanapata matokeo kutokana na aina ya wachezaji waliiopo.
“Yanga ni timu nzuri na yenye wachezaji wazuri, katika kikosi cha Yanga kuna wachezji wengi tu wazuri na wenye uwezo mkubwa wa kucheza mpira na kufanya maamuzi, kuna baadhi ya wachezaji tayari tunawafahamu na tumewafahamu kutokana na ubora wao.
“Mchezaji kama Aziz kina Mayele ni wachezaji ambao wana majina makubwa kwa sasa hivyo tumekuwa tukiwafuatilia kwa kuwa tunaamini kwa upande wetu tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuweza kupata matokeo tukiwa ugenini,” alisema kocha huyo.