Home Sports ROBERTINHO APATA DAWA YA RAJA CASABLANCA

ROBERTINHO APATA DAWA YA RAJA CASABLANCA

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo, kwa kuwaambia kuwa hataingia kivingine kimbinu watakapovaana dhidi ya Raja Casablanca ya nchini Morocco.

Hiyo ni baada ya kuanza vibaya hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa ugenini dhidi ya Horoya AC ya nchini Guinea wakifungwa bao 1-0.

Jumamosi hii, Simba watawakaribisha Raja Casablanca kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, ukiwa mchezo wa pili Kundi C katika michuano hiyo.

Akizungumza na Spoti Xtra, Robertinho alisema kuwa aina ya uchezaji ya ugenini na nyumbani kuna utofauti, hivyo atakavyocheza dhidi ya Casablanca anataka kuona vijana wake wakishambuliaji dakika zote 90 ili kuhakikisha anapata pointi nyumbani.

 

Robertinho alisema kuwa walipocheza dhidi ya Horoya aliwataka wachezaji wake kucheza kwa kujilinda na kushambulia kidogo kabla ya kufungwa bao hilo na kuwataka kufunguka kwa kulishambulia goli la wapinzani kwa lengo la kusawazisha.

 

Aliongeza kuwa, amepanga kuifanyia maboresho safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na John Bocco, Jean Baleke, Pape Sakho, Clatous Chama na Kibu Denis kuhakikisha wanapata ushindi wa mabao mengi nyumbani wakianza na Raja Casablanca.

 

“Ninataka kuona wachezaji wangu wakilishambulia goli la wapinzani wetu mara nyingi zaidi kwa maana ya dakika zote za kila mchezo tutakaoucheza nyumbani.

 

 “Katika hatua hii ya mashindano haya, kila timu inatakaiwa kupata ushindi nyumbani na ugenini kwenda kutafuta angalau sare.

 

 “Mchezo uliopita dhidi ya Horoya wachezaji wangu walicheza vizuri kwa kufuata maelekezo yangu ambayo ni kujilinda kwanza na kushambulia kwa kushitukiza, tulifanikiwa hilo licha ya kuruhusu bao moja.

 

 “Tunarejea nyumbani kujiandaa na mchezo wetu wa pili dhidi ya Raja Casablanca na kikubwa nimepanga kuifanyia maboresho safu ya ushambuliaji ambayo ilipoteza nafasi nyingi za wazi tukiwa ndani ya 18 tulipocheza na Horoya,” alisema Robertinho.

Previous articleSiku ya Redio Duniani Meridianbet Yapiga Hodi ITV & Radio One
Next articleHILI KUBWA LA M 5, MSIMBAZI WATOA SHUKRANI