MADRID NA KISHINDO FAINALI KOMBE LA DUNIA

HALI ya hewa hapa ni baridi kali lakini haizuii joto la mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Klabu kuwa juu.

Licha ya kwamba hakuna timu ya Morocco baada ya Wydad ambao ni mabingwa wa Afrika kutolewa mapema, bado hamu kubwa ya mashabiki ni kuiona Real Madrid.

Madrid watacheza fainali hiyo leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abellah baada ya kuitwanga vibaya Al Ahly ya Misri kwa mabao 4-1.

Al Hilal wao walianza kuamka dakika 88 ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Wydad, wasawazisha na mwisho wakashinda kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 30 za nyongeza.

Sasa wana mzigo ambao unahitaji mnyamwezi aweze kuufikisha, Real Madrid walionyesha kiwango cha juu sana dhidi ya Ahly.

Bahati nzuri hakukuwa na umakini wa juu katika kuzitumia nafasi zilizopatikana lakini ilionekana wazi ni timu ya kiwango tofauti na Ahly kutokana na aina ya uchezaji wao.

Mashabiki wengi wa Morocco wao hawakutaka kujificha tokea mwanzo, baada ya Wydad kutolewa wala hawakuwa na baya kwa Madrid.

Nakukumbusha kwa Madrid, mazingira ya Morocco kwa hali ya hewa na hata muonekano wa mazingira kwa asilimia 75 unafanana kabisa.

Maana yake hawawezi kuwa na shida hata kidogo kwa maana ya mazingira na watakuwa kama wako nyumbani ukilinganisha na Al Hilal.

Ukiachana na hivyo, hapa Rabat kuna tawi kubwa la mashabiki wa Real Madrid na linaweza kuwa ndio tawi kubwa zaidi kuliko jingine Afrika.

Hawa hujipanga kwenda uwanjani kwa wingi na inawezekana kabisa kuwa hakuna hata sababu ya Madrid kuleta mashabiki wake kutoka Hispania.

Nakukumbusha Madrid wameshabeba kombe hilo mara nne, kama watalibeba hii leo itakuwa mara tano na watakuwa wameandika rekodi mpya na bila shaka hili ndilo wanalolitaka.

Timu inayocheza na Madrid ni kati ya timu zinazokua kwa kasi katika soka la dunia na ndio vigogo wa soka la Asia kwa sasa na kama ulisikia walikuwa wakitaka kumsajili Lionel Messi.

Al Hilal watakuwa na kazi ngumu ya kuonyesha wanaweza kusimama na kuitangazia dunia tofauti na inavyojua kuhusiana na Madrid ambao wakiingia fainali, njaa yao huzidi kiwango na mapambano yao hayana mfano.

Andre Camilo, Moussa Marega, raia wa Mali huyo aliyewahi kukipiga FC Porto, Odion Ighalo raia wa Nigeria ambaye amecheza Watford na Manchester United za Premier League na Salem Adawsari ambaye anakumbukwa kwa kuifunga Argentina katika Kombe la Dunia Qatar ndio watakaotegemewa zaidi kuibeba Hilal katika mechi hiyo ngumu.

Katika soka hakuna lisilowezekana na kama Madrid watafanya uzembe basi kinaweza kuwatokea kitakachowashangaza kwa kuwa mara nyingi fainali huwa na yasiyotarajiwa kwa kuwa Hilal wamekuwa na nidhamu kubwa sana hasa katika eneo la ukabaji.

Madrid wanaonyesha hawataki mzaha, Kocha Carlo Ancelotti bila shaka anaonyesha hakufurahishwa sana na kiungo wake Camavinga ambaye alimchezesha kama beki wa kushoto na ndiye aliyesababisha penalti kwa kumkwatua Persi Tau, raia wa Afrika Kusini na Ahly ikapata penalti.

Kaongeza nguvu baada ya Militao kutua hapa juzi na akafanya mazoezi na wenzake. Pia mwamba Karim Benzema naye amejiunga na wenzake hapa Morocco.

Hii inaonyesha Madrid hawataki utani na inawezekana baadhi ya mapungufu ambayo ameyaona Ancelotti, basi anataka kuyarekebisha mapema kwa uhakika zaidi.

Gumzo la tiketi katika mji wa Rabat ni kubwa sana lakini gumzo hilo hata kwenye jiji kubwa la Casablanca na watu wengi sasa wanazitafuta tiketi kwa udi na uvumba.

Wako walio tayari kukununua tiketi hata Dilham 3,000 ya hapa ambayo ni dola 300 (takribani Sh milioni 1) ili kupata tiketi katika majukwaa ya kawaida tu kwenda kuishuhudia mechi hiyo ya kihistoria.

Hii ni fainali ya tatu ya Kombe la Dunia kuchezwa Morocco baada ya zile mbili za mwaka 2013 na 2017 lakini bado wapenda mpira wa Morocco wanachotaka kuingia kwenye historia. Wako wanataka kufikia hat trick ya fainali, wako wanataka kuwa na mbili na wengine wanapambana kwa kuwa ndio fainali ya kwanza wanaweza kupata nafasi.

Katika soka vigumu sana kutabiri matokeo mapema lakini bado unaweza kutoa nafasi kwa wale wenye kiwango bora zaidi.

Madrid wanaweza kuchukua asilimia 65 lakini bado kama Al Hilal watakuwa wamejipanga zaidi, wanaweza kubadili mchezo na mambo yakawa tofauti.