INAELEZWA kuwa, licha ya kuzungumzia mafanikio ya Jurgen Klopp ndani ya Liverpool, lakini mambo yanaweza kubadilika wakati wowote kikosini hapo na nafasi yake ikachukuliwa na kiungo wa zamani wa timu hiyo, Xabi Alonso.
Klopp raia wa Ujerumani, ndiye alibadili mambo na kuweka historia klabuni hapo baada ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufuta ukame wa miaka 30 kukosa taji la Premier League.
Kocha huyo kwa sasa ana mkataba mpaka 2026 na tayari alieleza hivi karibuni kuwa hana mpango wa kuondoka.
Lakini mambo yamekuwa magumu baada ya wikiendi iliyopita Liverpool kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la FA, wakiwa ni mabingwa watetezi, huku wakiwa nafasi ya tisa katika msimamo wa Premier League.
Taarifa kutoka kwa wachezaji na wakongwe wa klabu hiyo, zinaeleza kuwa Liverpool inamuangalia mchezaji wake wa zamani kwa ukaribu zaidi kuchukua mikoba ya Klopp.
Anayetajwa kwa sasa ni Xabi Alonso ambaye amefanikiwa kuibadili Bayer Leverkusen ambayo ilikuwa kwenye hatihati ya kushuka daraja Bundesliga na sasa ipo nafasi ya tisa, alitua kikosini hapo Novemba mwaka jana.
Ripoti zinaeleza kuwa, Liverpool wanamuangalia kwa ukaribu kocha huyo ambaye Steven Gerrard amekuwa akimkubali.
Awali Gerrard alikuwa akiitaka Liverpool kabla ya kupewa mikoba ya kuinoa Aston Villa ambayo hivi sasa ameachana nayo baada ya kutimuliwa.