>

MBAPPE ANAMTAKA BERNARDO PSG

STAA wa Ufaransa, Kylian Mbappe anataka PSG imsajili Bernardo Silva wa Man City ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji la klabu hiyo.

Mbappe anamtaka Silva kwenda kuungana naye Parc des Princes mwishoni mwa msimu huu.
Silva, 28, alimwambia Rob Dawson wa ESPN msimu uliopita wakati wa majira ya joto kwamba mustakabali wake ndani ya kikosi cha Pep Guardiola hauna uhakika sana. Hata hivyo, aliishia kusalia Etihad.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno alihamia Uingereza mwaka 2017 akitokea Monaco, ambako alikuwa mchezaji mwenza wa Mbappe, wakati huo akiwa kijana mdogo zaidi.

Wawili hao walikuwa wachezaji muhimu katika kikosi kilichoshinda taji la Ligue 1 2016-17 na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, na sasa mshambuliaji huyo wa PSG anaripotiwa kutumia ushawishi wake katika klabu hiyo kuungana na Silva katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Silva ana mkataba hadi 2025, kumaanisha kuwa City hawana shinikizo la kumuuza isipokuwa kwa ofa muhimu kama itatokea.