>

CHELSEA KUTEKETEZA TENA BIL 101

KLABU ya Chelsea wanajiandaa kutoa ofa ya kumsajili Malo Gusto wa Lyon, kwa Euro milioni 40 (Sh bil 101.4) kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za habari ikiwemo ESPN.

Hakuna ofa rasmi iliyotolewa na Chelsea kwa Gusto, lakini tayari amekubaliana na klabu hiyo kwa mkataba wa miaka sita na nusu na anataka kuhamia Stamford Bridge.

Lyon watajaribu kumrudisha kwa mkopo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 hadi mwisho wa msimu. Hata hivyo, Chelsea wanasita kukubaliana na kumtaka ajiunge nao mwezi huu.

Gusto, ni zao la Akademi ya Lyon ambaye pia amekuwa akihusishwa na Manchester United, alianza kuichezea klabu hiyo akiwa na umri wa miaka 17 na tayari amecheza mechi 47 za wakubwa kwenye kikosi cha kwanza.

Pia yuko kwenye rada za Didier Deschamps kwenda kutumikia timu ya taifa akiwa tayari ameiwakilisha Ufaransa katika kila ngazi ya umri mbalimbali.

Beki huyo wa pembeni ni hodari kwa kuanzisha mashambulizi na mwenye kasi kubwa na uwezo wa kupiga krosi, Gusto amebakiza takribani miezi 18 katika mkataba wake uliopo Lyon.