MARA baada ya kufikia makubaliano mazuri ya kuvunja mkataba na timu yake ya Yanga, kiungo Mrundi Gael Bigirimana amekubali yaishe na juzi Jumatatu mchana alipanda ndege kurejea nyumbani kwao Burundi.
Hiyo ni baada ya kufikia makubaliano mazuri ya pande mbili mchezaji na timu yake ya zamani ya Yanga iliyokubali kumlipa Sh 700Mil kwa awamu tatu.
Yanga imekubali kuvunja mkataba wa mwaka mmoja na nusu na kiungo huyo aliyewahi kuichezea Newcastle ya Uingereza.
Akizungumza na Championi Jumatano, Bigirimana alisema kuwa ameondoka kwa amani baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano mazuri ya kuuvunja mkataba wake huo.
Bigirimana alisema kuwa amerejea nyumbani kwao Burundi kwa ajili ya kujipanga na kuanza maisha na changamoto mpya huko anapokwenda.
Aliongeza kwa kuitakia kila la heri timu yake yake hiyo ya zamani, ikiwemo kupambania kutetea mataji yote ya msimu uliopita pamoja na kufika mbali kimataifa.
“Jana (juzi) nilianza safari ya kurejea nyumbani Burundi tayari kwa ajili ya kuanza maisha mapya mengine nje ya Yanga baada ya kudumu kwa muda mchache.
“Na nimeondoka Yanga baada ya kufikia muafaka mzuri na waajiri wangu ambao nimevunja nao mkataba wa mwaka mmoja na nusu.
“Nimeondoka huku nikiamini ipo siku moja nitarejea tena kuichezea Yanga baada ya kukutana na changamoto katika kipindi nilichokuwepo hapo,” alisema Bigirimana.