CHAMA ANAIWAHI COASTAL UNION

CLATOUS Chama, kiungo mshambuliaji wa Simba kuna asilimia kubwa akaibuka kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union ambao ni wa Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kuchezwa Januari 28, Uwanja wa Mkapa, Dar.

Chama hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichoshuhudia ubao wa Uwanja wa Jamhuri ukisoma Dodoma Jiji 0-1 Simba kwa bao la Jean Baleke kwa kile kilichoelezwa kuwa anaumwa Malaria.

Ikumbukwe kwamba wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 3-2 Mbeya City Januari 18 ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa Kocha Mkuu, Roberto Oliveira, Chama aliyeyusha dakika 33 na alitoa pasi moja ya bao nafasi yake ikachukuliwa na Pape Sakho.

Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Simba, Ahmed Ally alisema kuwa hali za wachezaji wao zinazidi kuimarika.

“Maendeleo kwa sasa ni mazuri kwa wachezaji wetu ambao hawakuwa kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ikiwa ni pamoja na Clatous Chama, Moses Phiri, Henock Inonga na Peter Banda na kuna uwezekano wakawa miongoni mwa wachezaji watakaokitimua ikiwa watakuwa fiti kwa mujibu wa ripoti ya daktari,” alisema Ally.