BEKI mpya wa Yanga raia wa Mali, Mamadou Doumbia ametamka kuwa yeye sio mtu wa maneno mengi, na mashabiki wasubirie kuona mazuri kutoka kwake.
Hiyo huenda ikawa kama salamu kwa washambuliaji wa wapinzani wao, Simba akiwemo mpya Mkongomani Jean Baleke, Moses Phiri na nahodha John Bocco.
Doumbia ni kati ya wachezaji watatu wapya waliosajiliwa na timu hiyo, katika dirisha hili dogo wengine ni kiungo Mudathir Yahya, mshambuliaji Kennedy Musonda na kipa Metacha Mnata.
Kwa mujibu wa Doumbia amesema kuwa ana furaha kubwa kuichezea Yanga ambayo nchini kwao Mali inafuatiliwa kwa karibu tofauti na nyingine za hapa nchini.
Doumbia alisema kuwa amekuja kufanya kazi Yanga, na kikubwa kuipa mataji yote wanayoyatetea katika msimu huu pamoja na kufika mbali katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Aliongeza kuwa kikubwa anahitaji sapoti kubwa ya wachezaji na mashabiki katika kuhakikisha anaipambania Yanga kwa kuanzia mzunguko huu wa pili wa ligi.
“Kwanza kabisa nimefurahi sana kufika hapa, Yanga ni klabu kubwa sana kule nyumbani kwetu Mali, kwani ni timu inayofuatiliwa na watu wengi, hivyo kuja hapa ni jambo kubwa sana kwangu kama mchezaji.
“Mimi sio mtu wa maneno sana, kazi yangu ni uwanjani na mashabiki wategemee mazuri kutoka kwangu. Nawapenda sana.
“Nafahamu hapa Yanga nitakuta ushindani mkubwa, lakini nitajitahidi kupambana kuingia katika kikosi cha kwanza, licha ya kuwakuta mabeki wengine hapa,”alisema Doumbia.