YACOUBA NA YANGA, MAISHA LAZIMA YAENDELEE

ALIKUWA moja ya wachezaji tegemeo ndani ya kikosi cha Yanga kwenye eneo la ushambuliaji ambapo aliunda pacha nzuri na Deus Kaseke.

Yacouba amewaaga mabosi wa timu hiyo na kuwashukuru kwa muda ambao alikuwa nao ndani ya kikosi hicho.

Alikuwa nje kwa muda wa msimu mzima akipambania hali yake baada ya kupata maumivu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shootig.

Yanga walionyesha uungwana kwa kumgharamia mchezaji kwa muda ambao alikuwa hajarejea kwenye ubora wake na kwa sasa yupo fiti anarejea mdogomdogo.

Kwenye Kombe la Mapinduzi alipewa nafasi ili aonyeshe makeke yake lakini hakuwa katika ubora wake.

Nasreddine Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga alikuwa anamtazama kwa karibu mshambuliaji huyo lakini haijawa vile alivyotarajia.

Yanga wameshukuru Yacouba na Yacouba amewashukuru Yanga, maisha lazima yaendelee.

Yacouba ameandika:”Ulikuwa wakati mzuri tangu tulipokuwa pamoja mpaka sasa asanteni kwa upendo wenu kwangu na ushirikiano wenu kwanzia kwa wachezaji hadi uongozi wote wa Yanga na mashabiki daima nitawakumbuka hadi wakati mwingine wananchi asante sana na kwaherini nawapenda,”.