UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa kwa sasa unawekeza nguvu zao zote kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la Azam Sports Federation ambalo wanashiriki.
Timu hiyo ilienguliwa kwenye Kombe la Mapinduzi 2023 kwa kugotea hatua ya nusu fainali baada ya ubao wa Uwanja wa Amaan kusoma Azam FC 1-4 Singida Big Stars, Januari 8.
Januari 13,2023 walishuhudia bingwa mpya akipatikana kwenye fainali za Kombe la Mapinduzi.
Ni Mlandege ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Big Stars.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulakalim Amin alisema kuwa kazi bado inaendelea kwenye mashindano ambayo wanashiriki.
“Bado kuna mashindano ambayo tunashiriki ikiwa ni kwenye ligi pamoja na Kombe la Shirikisho hapa ushindani ni mkubwa nasi tunaongeza nguvu zaidi.
“Kikubwa ni kuona kwamba kila mechi ambayo tunacheza tunapata matokeo hilo linawezekana kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kutafuta matokeo,” alisema.