MWENDO wa Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi 2023 umegota mwisho baada ya kuambulia sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Singida Big Stars.
Yanga ambayo ipo kundi B la Mapinduzi 2023 ilikuwa inahitaji ushindi ili kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali lakini haikuwa hivyo kwani hata Singida Big Stars nao walikuwa wanahitaji ushindi.
Mabao yote mawili yalipatikana katika dakika 45 za mwanzo kutokana na mapigo huru huku ukipigwa mpira wa ushindani kwa miamba hao wawili.
Ni Francis Kazadi alianza kuipa bao Singida Big Stars dakika ya 22 akimalizia pigo la kona ambalo lilitemwa na kipa Johora Eric kisha Yanga walisubiri mpaka dakika ya 31.
Beki wao David Bryson ambaye alikuwa sababu pia ya kupata ushindi kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya KMKM alipiga pigo la faulo iliyoleta bao katika mchezo huo.
Ikumbukwe kwamba mbele ya KMKM Bryson alipiga faulo dakika ya 90 iliyokuwa chonganishi kwa wapinzani wao na ilifanikiwa kuleta bao la ushindi lililofungwa na Dickson Ambundo.
Kwa matokeo hayo ya Yanga kuvuna pointi moja kwenye kundi B inafikisha pointi nne sawa na Singida Big Stars kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungana.
Sasa Singida Big Stars itamenyana na Azam FC hatua ya nusu fainali na nusu fainali nyingine itawahusisha waliowavua ubingwa Simba, Mlandege dhidi ya Namungo iliyokuwa kundi D.
Shukrani kwa kipa wa Singida Big Stars, Benjamin Haule ambaye aliokoa hatari nyingi langoni mwake na kuifanya timu hiyo kupata pointi moja katika mchezo huo.
Sasa Yanga inaungana na watani zao wa jadi Simba kuwa watazamaji wa kombe hilo ambalo limekuwa na ushindani mkubwa mwaka huu 2023.