MARA baada ya kutambulishwa Yanga, kiungo mkabaji, Mudathir Yahya, amesema malengo yake ya kwanza ni kupambania namba ili aingie katika kikosi cha kwanza.
Kiungo huyo ni mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Yanga katika dirisha hili dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 16, 2022 na kutarajiwa kufungwa Januari 15, 2023.
Mudathir ana kibarua kigumu cha kuwania namba mbele ya Khalid Aucho, Gael Bigirimana na Zawadi Mauya ambao wote wanacheza namba 6.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mudathir alisema kikubwa kwake ni uzima pekee, kwani anaamini kiwango bora alichonacho ndani ya uwanja atapata nafasi ya kucheza.
Mudathir alisema kikubwa atakachokifanya hivi sasa ni kumshawishi kocha wa kikosi hicho, Mtunisia, Nasreddine Nabi kwa kumuoneshea uwezo wake kila atakapompa nafasi ya kucheza.
“Kwa kipindi chote nikiwa sina timu ya kuichezea, nilikuwa nafanya mazoezi hapa Zanzibar, hivyo nipo fiti na tayari kuichezea Yanga kwa kuanzia Kombe la Mapinduzi.
“Nafahamu ushindani uliokuwepo hivi sasa wa namba, lakini hiyo hainifanyi niogope na badala yake nitahakikisha ninapambana ili niingie katika kikosi cha kwanza,” alisema Mudathiri