Home Sports 2022 IMEGOTA UKINGONI,2023 IWE YEYE FURAHA

2022 IMEGOTA UKINGONI,2023 IWE YEYE FURAHA

TAYARI mwaka 2022 umemalizika na tumeingia mwaka 2023, kulikuwa na matukio mengi kwenye dunia ya soka mazuri na mabaya ambayo kwa kiasi kikubwa yaliibua mijadala mikubwa kwa wanafamilia wa mpira wa miguu nchini.

Natarajia kuona mabadiliko makubwa kwenye soka letu katika nyanja zote kuanzia utawala, uendeshaji pamoja na utendaji ili tuendelee kuona soka letu likipiga hatua.

Sitarajii kuona mambo ambayo hayatakuwa na tija kwe nye mpira wetu.

Nizipongeze timu zote ambazo zilikuwa na mwenendo bora kwa mwaka 2022 tunatarajia muendeleze pale mlipoishia kwa mwaka huu.

Kwa timu za Simba na Yanga ambazo zinakwenda kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa mnapaswa kutambua kuwa mmebeba jukumu zito la kutetea nafasi nne za nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Ni matarajio ya wengi kuona mnafika mbali kuanzia hatua ya nusu fainali na ikiwezekana hatua ya fainali kama walivyofanya Simba mwaka 1993. Wachezaji mnapaswa kutambua kuwa mna jukumu kubwa la kuzipambania nembo za timu zenu.

Kwa upande wa timu ambazo zinaendelea na harakati za usajili wa dirisha dogo hakikisheni usajili unaofanyika unazingatia matakwa ya benchi la ufundi na usiwe kwa ajili ya kufurahisha kundi la watu wachache ambao wanaangalia zaidi maslahi yao binafsi.

Hiki siyo kipindi cha kuona kuna migogoro ya hapa na pale ambayo ni wazi kwa kiasi kikubwa inaharibu taswira ya soka letu ambalo tunajinasibu kila leo kuwa limepiga hatua kubwa.

Mwaka 2022 ulikuwa wa neema kwa timu za Ligi Kuu Bara kwani ni kipindi ambacho Azam waliweka fedha nyingi kwenye mpira wetu jambo ambalo limeenda kumaliza kwa kiasi fulani tatizo la uchumi kwa timu nyingi za madaraja ya kati. Ni kipindi ambacho hatukuwahi kusikia tatizo la mishahara wala shida za usafiri kwenye timu hizi.

Hivyo basi mnatakiwa kuendeleza ubora uwanjani ili wadhamini wazidi kushawishika na kuweka fedha zao kwa kiasi kikubwa ili tuweze kufaidi soka halisi la ushindani na siyo soka la maigizo na hadithi za Bulicheka.

Wachezaji ambao hamkuwa na nyakati bora mwaka jana na hamkupitiwa na panga la usajili huu ni mwaka wenu kujitafakari upya na kuona ni wapi mlikuwa na mapungufu ili muweze kuboresha kwa ajili ya kuzitumikia timu zenu.

Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi kwa Klabu ya Simba na tayari mchakato unaendelea wa kuwapata viongozi wapya ambao wataendeleza gurudumu la klabu hiyo hivyo ni muda sahihi kwa wanachama na mashabiki wa Simba kuwa watulivu na kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya manufaa ya timu yenu hapo baadae.

Hivi karibuni tumeona sarakasi zikianza kwa baadhi ya wagombea ambao ni wazi wameona hawakutendewa haki wengine wakikata rufaa na wengine wameamua kuacha lipite niwaombe tu kwa sasa mnapaswa kuangalia zaidi maslahi ya timu yenu kuliko haya mnayoendeleza hivi sasa.

Bila shaka yoyote mpira wetu unazidi kupiga hatua hivyo tunatakiwa kuendeleza kwenye ubora na kuboresha kwenye mapungufu ili tuzidi kujitangaza kimataifa zaidi.

Mwisho 2022 ulikuwa mwaka wa neema kwa timu zetu za taifa kama timu ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 ambayo ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza

Pia timu ya taifa ya walemavu nayo ikifanya vizuri kwenye fainali za kombe la Dunia zilizofanyika nchini Uturuki. Happy New Year ikawe kheri kwetu.

Previous articleYANGA KAMILI KUIKABILI KMKM
Next articleKIUNGO WA KAZI AONGEZA MKATABA YANGA