YANGA HAWANA BAHATI NA SOPU ANAWATUNGUA TU

ABDUL Suleiman, ‘Sopu’ nyota wa Azam FC nyota yake huwa inawaka anapopata nafasi ya kucheza dhidi ya Yanga.

Nyota huyo amefanikiwa kuifunga Yanga mabao matano huku yote akimtungua kipa mmoja Diarra Djigui.

Sopu alianza kufanya hivyo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho ambao ulikuwa ni wa fainali akiwa ni mchezaji wa kwanza kufunga hat trick kwenye fainali.

Zama hizo alikuwa ndani ya Coastal Union ya Tanga chini ya Kocha Mkuu Juma Mgunda ambaye kwa sasa anainoa Simba.

Sopu alifunga hat trick na kusepa na mpira kwenye sare ya kufungana mabao 3-3 lakini timu hiyo ilikwama kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa kupoteza kwa kufungwa penalti 4-1.

Alipoibukia ndani ya Azam FC, Sopu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Azam FC 2-3 Yanga alitupia mabao mawili.

Nyota huyo anashikilia rekodi ya kuwa mzawa aliyemtungua mabao mengi mdaka mishale wa Yanga, Diarra ambaye ana tuzo ya kipa bora kwa msimu wa 2021/22.

Ikumbukwe kwamba Sopu ana tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho pamoja na kuwa mfungaji bora pia.