AZAM FC HAWANA BAHATI NA MAYELE

AZAM FC hawana bahati na Fiston Mayele kwa kuwa kwenye mechi ambazo atawatungua lazima wayeyushe pointi tatu mazima.

Kwenye mchezo wa kwanza mzunguko wa kwanza msimu wa 2022/23, kwenye sare ya kufungana mabao 2-2 , Mayele hakufunga kwa Azam FC bali ni kiungo mzawa Feisal Salum alimtungua mabao yote mawili Ali Ahamada.

Ikumbukwe kwamba kwa msimu wa 2021/22 wakati ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Azam FC 1-2 Yanga bao la ushindi mtunguaji alikuwa ni Mayele dakika ya 77.

Msimu huu pia mzunguko wa pili Desemba 25 2022 wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Azam FC 2-3 Yanga, Mayele alitupia bao moja dakika ya 31.

Lile la ushindi lilitupwa kimiani na Farid Mussa dakika ya 77 na kuipa pointi tatu mazima Yanga ambao ni vinara wa ligi wakiwa na pointi zao 47 baada ya kucheza mechi 18.

Azam FC wapo nafasi ya tatu kibindoni wana pointi 37.