HIZI HAPA MASHINE ZA KAZI YANGA KWA AJILI YA KUIMALIZA AZAM FC

BENCHI la ufundi la Yanga limeweka wazi kuwa wachezaji wao wote ikiwa ni pamoja na Fiston Mayele mwenye mabao 13 na pasi moja, kiungo Aziz KI mwenye pasi tatu za mabao na mawili wanaandaliwa kuwakabili Azam FC.

Mbali na hao pia kwenye safu ya ulinzi Yannick Bangala mwenye mabao mawili, Dickson Job ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuanza kikosi cha kwanza.

Cedrick Kaze, kocha msaidizi wa Yanga amesema kuwa wamekuwa wakiwapa mapumziko wachezaji hao kwa ajili ya mchezo dhidi ya Azam FC.

“Ukiangalia kwenye ratiba yetu tumekuwa na mechi zinazofuatana tumetoka kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho kisha tukawa na mechi nyingine mbele halafu tuna mchezo dhidi ya Azam FC hapo ni lazima tuwape muda wa mapumziko wachezaji.

“Imekuwa hivyo kwenye mechi zetu ambazo zimepita kama uliona kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union Mayele hakumaliza mchezo na ilikuwa hivyo hata tulipocheza na Polisi Tanzania Aziz hakumaliza dakika zote.

“Tunataka wachezaji wapate muda wa kupumzika pamoja na kurejea kwenye ubora kwa mechi zile ambazo zinafuata hivyo tunazidi kujipanga kuendelea kupata matokeo,” amesema Kaze.

Leo Desemba 25,2022 Yanga ina kibarua cha kusaka pointi tatu dhidi ya Azam FC mchezo unoatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.