>

WAKATI WENU SASA KIMATAIFA SIMBA, YANGA

TAYARI makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika yamewekwa hadharani huku wawakilishi wetu Simba na Yanga wakiwafahamu wapinzani wao ambao watachuana nao kuisaka hatua ya robo fainali ya mchuano hiyo.

Simba wamepangwa na timu za Horoya, Raja Casablanca na Vipers huku Yanga wakiwa kundi moja na miamba Real Bamako, TP Mazembe na timu ya US Monastri  ukitazama makundi haya unaona ni makundi ambayo wawakilishi wetu wanapaswa kufanya maandalizi ya kutosha ili kufikia malengo yao.

Kwa sasa tunaelekea katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo huu ni wakati sahihi kwa timu hizi kuanza kufanya maboresho ya kina kwenye vikosi vyao ili kuleta ushindani wa kweli kwenye michuano hii na si kuishia kuwa wasindikizaji.

Kwa misimu minne mfululizo Simba wamepambana kuiwakilisha vyema nchi jambo lililopelekea Tanzania kupata nafasi ya kuingiza timu nne kwenye michuano hii baada ya kuingia hatua ya makundi mara tatu na hatua ya robo fainali mara tatu.

Simba na Yanga mnapaswa kulifanya hili la timu nne kimataifa kuwa jambo la mazoea kwenye soka letu hivyo ni wajibu wenu kupambana kufika mbali kwenye michuano hii ili tusiziweke rehani nafasi nne kimataifa.

Viongozi huu ni wakati wa kuanza kupanga mikakati sahihi ya kuzivusha timu zenu kufika hatua za mbali kwenye michuano hii huu siyo wakati wa kujikita kwenye mambo ambayo hayana tija na maendeleo ya timu zenu.

Ni matamanio ya kila Mtanzania mpenda maendeleo kwenye soka kuona timu zetu zinatoboa kuanzia hatua ya Nusu fainali na ikiwezekana fainali kwani kama Simba waliweza kufika fainali mwaka 1993 pia inawezekana hivi sasa kuona Yanga na Simba wanaleta taji la Afrika na Shirikisho nchini.

Timu zote zimesheheni wachezaji wa viwango vya juu ambao ni wazi wakiamua kwa nia ya dhati kumwaga jasho lao kwa ajili ya nembo za timu zao ninaamini wanaweza kuandika historia iliyotukuka kwenye mpira wetu.

 Kama Yanga waliweza kufanya maajabu pale Tunis dhidi ya Club African, Simba wakawashangaza AS Vita pale Kinshasa ni wazi wachezaji wakiweka nia ya dhati lolote linawezekana.

Wakati ni sasa hamtakiwi kubaki kuwa timu za kushiriki pekee bali mnapaswa kuwa timu shindani ambazo hakuna timu itakayokuwa ikitamani kupangwa nanyi kundi moja. Lakini haya yote yatawezekana ikiwa tu mtaamua kujikita kwenye weledi na kuachana na siasa za hovyo na propaganda ambazo miaka nenda rudi haziwafaidishi chochote kwenye maendeleo ya timu zenu.

Nitoe rai kwa wale mashabiki oyaoya ambao wamekuwa mashabiki matokeo pekee huu ndiyo wakati wenu kuhakikisha mnakuwa pamoja na timu zenu katika kila nyakati na si kusubiri timu inapopata matokeo ndiyo mjitokeze na pale mambo yanapoharibika mnageuka mashabiki lawama.

Zile tabia za kuandamana pale Uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK Nyerere kupokea wageni wanaokuja kucheza na timu zinazokuja kucheza na watani zenu hampaswi kuziendekeza hivyo ni wajibu wenu kuwekeza nguvu hizi kwenye kuzisapoti timu zenu kuhakikisha zinafanya vizuri kimataifa.