>

SUALA LA KUSHUKA DARAJA LIPO, TIMU ZIKUMBUKE HILI

MWANZO siku zote ni wakati wa kutengeneza mwisho kwenye mpango kazi ambao unafanyika hivyo kwa sasa ni maandalizi kwa ajili ya kukamilisha ligi msimu wa 2022/23.

Tunaona kuna timu ambazo ushindani wake umekuwa ni wa kawaida wakiamini kwamba wataendelea kucheza ligi hii muda wote hata msimu ukiisha.

Kwa wale ambao wanafikiria hivyo kwa sasa ni muhimu kushtuka na kubadili gia kwani ligi ipo mzunguko wa kwanza ambao unakaribia kugota ukingoni.

Kukaribia kugota ukingoni ina maana kwamba mzunguko wa pili unakuja ambapo maamuzi yatatolewa mwisho nani atasepa na ubingwa na timu ipi itashuka daraja.

Kwenye makaratasi kuna timu zimesajili wachezaji wazuri lakini kwenye uhalisia hawawapi yale matokeo ambayo wengi wanatarajia hivyo ni muhimu kulitazama hili kwa umakini.

Wachezaji wanapaswa kutambua kwamba muda hausubiri unasonga mbele na kushindwa kupata matokeo ndani ya dakika 90 ni mwanzo wa kutengeneza mwisho mbaya.

Ili kuwa na mwisho mzuri kwenye ligi ni lazima matokeo yapatikane hivyo kwa sasa muhimu kila mchezaji kulitambua hilo kama alikuwa amesahahau.

Benchi la ufundi kuna umuhimu wa kubadili mbinu za ushindi ikiwa zile ambazo zimekuwa zikitumika zinafeli hii itawafanya wachezaji kuwa na mbinu mpya kwenye ushindani.

Kila kitu kinawezekana hivyo ikiwa hakutakuwa na mpango kazi wa kupata matokeo mazuri kwa sasa basi kutakuwa na mpango kazi wa kujiandaa kushuka wakati ujao.