MGUNDA:MBEYA CITY NI WAGUMU

JUMA Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa aliweka wazi tangu awali kuwa mchezo wao dhidi ya Mbeya City utakuwa mgumu na matokeo ambayo wamepata yametokana na ushindani huo.

Licha ya kupata bao la kuongoza dakika ya 14 Simba iliokota bao dakika ya 78 kupitia kwa Tariq Seif ambaye alifanya mpango wa timu hiyo kusepa na pointi tatu kukwama ugenini, Uwanja wa Sokoine.

Mgunda amesema:”Nilisema tangu awali kwamba Mbeya City ni timu ngumu na imekuwa hivyo licha ya kwamba tulipata bao la mapema kipindi cha kwanza haikuwa hivyo kwetu mwisho wao wakapata bao pia.

“Ambacho kimetokea ninaweza kusema ni makosa ya safu ya ulinzi lakini siwezi kuwapa lawama wachezaji wangu kwani wamepambana kwa kadri ya wanavyoweza na mwisho tumepata pointi moja ni sehemu ya matokeo,” amesema.

Mchezo ujao kwa Simba ni dhidi ya Polisi Tanzania unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Ushirika, Moshi Novemba 27.

Kikosi kwa sasa kimerejea Dar kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Simba imecheza mechi 13 ipo nafasi ya tatu na pointi zake kibindoni ni 28 vinara ni Yanga wenye pointi 29 baada ya kucheza mechi 11.