YANGA KAMILI KUIVAA DODOMA JIJI

KUELEKEA mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Bara kati ya Dodoma Jiji dhidi ya Yanga, benchi la ufundi la Yanga limeweka wazi kuwa kila kitu kipo sawa.

Ni Nasreddine Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa namna ambavyo wanapata ushindi na kutopoteza mchezo morali na ari ya kupambana inaongezeka kutokana na mashabiki kushangilia.

“Ni kitu kizuri watu wanahamasika na kushangilia rekodi yetu ya kutokupoteza mchezo, inatupa morali ya kuzidi kupambana kushinda mechi nyingi zaidi.
“Kuhusu Uwanja wa Liti kwa kweli hapa Singida wamejitahidi licha ya kuwa haupo bora kwa asilimia 100 wanastahili pongezi uwanja ni mzuri,”.

Yanga imecheza jumla ya mechi 47 bila kufungwa ndani ya ligi tangu ilipopoteza mbele ya Azam FC kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Mkapa msimu wa 2021/22.

Leo kikosi cha Yanga kimefanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo wa kesho na miongoni mwa wachezaji waliokuwa kwenye kikosi hicho ni Bakari Mwamnyeto, Aboutwalib Mshery, Sure Boy na Clement Mzize.