ISHU YA CHAMA KUFUNGIWA SIMBA YAJA NA JAMBO HILI

JUMA Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo dhidi ya Singida Big Stars huku akiwakosa nyota mbalimbali kutokana na sababu kadhaa.

Miongoni mwa nyota hao ni pamoja na kiungo chaguo namba moja la Mgunda, Clatous Chama ambaye amefungiwa kucheza mechi tatu kutokana na kosa la kushindwa kusalimiana na wachezaji wa timu pinzani.

Tukio hilo lilifanyika Oktoba 23, kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga. Mgunda amebainisha kuwa taarifa hiyo ameipata huku akioma wenye mamlaka wanapotoa maamuzi kuwafikiria na walimu wa timu.

“Wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Singida Big Stars, unajua ni moja ya timu ngumu ambazo zinashiriki ligi lakini ambacho ninaweza kusema maandalizi yamekamilika.

“Wapo wachezaji ambao tutawakosa ikiwa ni pamoja na Jimson Mwanuke, Israel Mwenda hawa bado hawajawa fiti lakini kwa upande wa Clatous Chama tumepata taarifa zake tunaheshimu maamuzi.

“Lakini ushauri kwa wenye mamlaka kama taarifa walikuwa nayo baada ya kikao Novemba 4 kisha tunapewa siku moja kabla ya mchezo wanapaswa kutufikiria na sisi walimu pia, haina maana nawapinga hapana ninaheshimu maamuzi yao lakini ukweli huwa ninapenda kusema,”.

Miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wapo kwenye kikosi hicho ni pamoja na Mzamiru Yassin, Joash Onyango, Kenned Juma, Erasto Nyoni na Sadio Kanoute.